Trump: Ukweli, Marekani inachukiwa sana duniani
Donald Trump, mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais Marekani utakaofanyika nchini humo siku chache zijazo, amesema, nchi hiyo inachukiwa sana duniani.
Trump ameyasema hayo huku akiashiria hatua ya Ufilipino kutangaza kukata uhusiano wake na Washington na kusema kuwa, ukweli ni kwamba Marekani inachukiwa duniani. Amesema kama ninavyomnukuu: "Ulimwengu unamchukia rais wetu, ulimwengu unatuchukia. Wenyewe mmeona kilichotokea Ufilipino baada ya miaka mingi. Wameamua kuelekeza macho yao kwa Russia na China." Mwisho wa kunukuu. Itakumbukwa kuwa Alkhamis iliyopita na katika ziara yake nchini China, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino alitangaza kujitenga nchi yake na Marekani katika uga wa kisiasa na kiuchumi.
Rais Duterte aliongeza kwa kusema: "Ninamaanisha kwamba, nimekubaliana na idolojia zenu na inawezekana nikafanya safari pia nchini Russia kwa ajili ya kuzungumza na Rais Vladmir Putin wa nchi hiyo." Mwisho wa kunukuu. Kufuatia hatua hiyo, mgombea wa chama cha Republican nchini Marekani amesema kuwa, hatua ya Ufilipino kujitenga na Washington inaashiria udhaifu wa hali ya juu wa Marekani katika uwanja wa kimataifa. Alisema kama ninavyonukuu: "Marekani imekuwa dhaifu sana kiasi cha kuifanya serikali ya Manila ambayo daima ilikuwa rafiki wa Washington kujitenga nasi." Mwisho wa kunukuu.