Ayatullah Khatami amtahadharisha Rais mteule wa Marekani kuhusu siasa za vitisho
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo katika mji wa Tehran amesema kuwa taifa la Iran halitaiamini serikali yoyote inayoingia madarakani huko Marekani.
Ayatullah Ahmad Khatami amesema katika hotuba za Swala hiyo kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Marekani hayabadili chochote katika siasa za kimabavu za nchi hiyo mbele ya mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, taifa la Iran kamwe haitasalimu amri mbele ya matakwa ya serikali zinazoingia madarakani nchini Marekani.
Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amemtahadharisha rais mteule wa Marekani kuhusu taathira mbaya za utekelezaji wa siasa za kutumia vitisho na uchokozi dhidi ya Iran na kueleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itapambana na kusimama kidete dhidi ya siasa hizo.
Ayatullah Khatami amesisitiza kuwa, walimwengu wamechoshwa na siasa za chokochoko na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika nchi zao na amemnasihi rais mteule wa nchi hiyo kuwa ni vyema ashughulikie matatizo mbalimbali ya watu wa nchi hiyo badala ya kuendeleza siasa za kichochezi dhidi ya nchi nyingine.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema mgombea wa kiti cha urais huko Marekani amekiri kwamba madeni makubwa ya nchi hiyo yameifanya Marekani ikaribie kufilisika na kuongeza kuwa: Ghasia na na ukosefu wa amani nchini humo vimeshtadi kiasi kwamba kila mwaka raia wengi hususan Wamarekani weusi huwa wahanga wa utumiaji mabavu unaojiri nchini humo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khatami ameashiria ombi la baadhi ya nchi kwa Marekani wakiitaka nchi hiyo isaidie kutatua migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa, nchi ambayo yenyewe haiwezi kutatua matatizo yake ya kiusalama na kifedha kamwe haiwezi kusadia katika suala la usalama wa eneo hili.