Kukasirishwa nchi za Magharibi na uamuzi wa Russia wa kujitoa ICC
Hatua ya Russia ya kutangaza kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imezikasirisha nchi za Magharibi za Ulaya na Marekani.
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya alisema siku ya Alkhamisi kuwa, amesikitishwa na uamuzi wa Russia wa kujitoa katika mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Amesema, Umoja wa Ulaya uliitaka kwa mara kadhaa Russia isijitoe katika mkataba wa Roma iliotiwa saini tarehe 13 Septemba 2000. Mkataba huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2002 ndio msingi wa kazi za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Naye John Kirby, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema kuwa, ijapokuwa nchi za dunia ziko huru kuamua kubakia au kutobakia kwenye mktaba huo, lakini jambo hilo halina maana kuwa mahakama hiyo haina faida. Matamshi hayo ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani yametolewa wakati nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa yaliyojitoa miaka mingi nyuma katika mahakama ya ICC.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hasira za nchi za Magharibi kwa uamuzi wa Russia wa kujitoa kwenye mahakama ya ICC unatokana na kuwa, hatua hiyo itazizuia nchi za Magharibi au Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kali za kukabiliana na maamuzi ya Russia kuhusu mgogoro wa Ukraine hususan suala la kujiunga na Russia eneo la Crimea. Weledi hao wa mambo wanaamini pia kuwa, mgogoro wa Ukraine ndio ulioifanya Russia iamue kujitoa katika mahakama ya ICC. Siku ya Jumatano, tarehe 16 Novemba, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema baada ya Kamati ya Haki za Binadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa, harakati za Russia katika eneo la Crimea ni kinyume cha sheria kwamba, Moscow, itajitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Baada ya hapo, Putin alikubaliana pia na pendekezo la Wizara ya Mahakama ya Russia la kujitoa nchi hiyo katika Mkataba huo wa Roma. Mkataba wa Roma ulipasishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1998 kwa kushirikiana na Russia katika mkutano uliofanyika mjini Rome, Italia. Mwaka 2000, Russia ilitia saini mkataba huo.
Kamati ya Haki za Binadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni ilipasisha muswada mmoja kwa kura 73 za kukubali na 23 za kukataa ambao unaituhumu Russia kuwa inawabagua wakazi wa eneo la Crimea wakiwemo Waukrain na makabila mengine kama ya Watatari, kama ambavyo pia muswada huo ulisema, Russia inalikalia kwa mabavu eneo la Crimea la Ukraine. Kazi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini Hague Uholanzi ni kufuatilia mashtaka ya mauaji ya umati, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. Tab'an, Russia haikusema rasmi kuwa sababu iliyoifanya kujitoa katika mahakama ya ICC ni msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala la kujiunga na Russia eneo la Crimea, bali imesema kuwa, utendaji mbovu wa mahakama ya ICC ndio ulioifanya Moscow ichukue uamuzi huo. Kwa mtazamo wa Moscow, ijapokuwa mahakama ya ICC ilianza kazi zake kwa ajili ya kuleta amani na usalama duniani, lakini imeshindwa kufikia malengo yake hayo.
Ijapokuwa nchi za Magharibi za Ulaya na Marekani zinailaumu Russia kwa kujitoa kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC, lakini swali linalojitokeza hapa ni kuwa, kama kweli uanachama wa nchi kubwa duniani katika mahakama hiyo ni jambo la dharura, kwa nini Marekani hadi hivi sasa inakataa kurejea kwenye mahakama hiyo? Ikumbukwe kuwa, Marekani iliamua kujitoa katika mahakama ya ICC miaka 14 iliyopita. Mwaka 2002, Marekani ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na kutangaza kujitoa kwenye mahakama hiyo ya kimataifa. Uamuzi huo ulichukuliwa na Washington wakati Marekani ilipokuwa inafanya mashambulizi ya kikatili nchini Afghanistan, na baada ya hapo wanajeshi wa Marekani wakaivamia Iraq. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika mahakama ya ICC mwaka 2002 ulichukuliwa ili kuwapa uhuru wanajeshi wa Marekani kufanya jinai zozote wanazopenda bila ya kuwa na woga wa kufuatiliwa kisheria na mahakama hiyo ya kimataifa.