Waislamu Marekani walaani hujuma ya 'kigaidi' Ohio
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20437-waislamu_marekani_walaani_hujuma_ya_'kigaidi'_ohio
Viongozi wa Kiislamu nchini Marekani wamelaani vikali kile vyombo vya usalama vimetaja kuwa hujuma ya kigaidi katika jimbo la Ohio, ambapo mwanafunzi mmoja wa Marekani mwenye asili ya Somalia aliwashambulia kwa kisu wanachuo wenzake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2016 10:41 UTC
  • Waislamu Marekani walaani hujuma ya 'kigaidi' Ohio

Viongozi wa Kiislamu nchini Marekani wamelaani vikali kile vyombo vya usalama vimetaja kuwa hujuma ya kigaidi katika jimbo la Ohio, ambapo mwanafunzi mmoja wa Marekani mwenye asili ya Somalia aliwashambulia kwa kisu wanachuo wenzake.

Taarifa ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani CAIR imelitaja tukio hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Ohio kama la kuhuzunisha na la kuvunja moyo.

Jana Jumatatu, kijana wa Kisomali kwa jina Abdul Razak Ali Artan mwenye umri wa miaka 18, aliwakanyaga kwa makusudi wapita njia kwa gari lake katika jimbo la Ohio, kabla ya kuingia katika chuo kikuu cha jimbo hilo na kujeruhi watu 11 kwa kuwadunga kisu.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani CAIR

Hata hivyo mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Ohio ambaye alikuwa mkimbizi kutoka Somalia, aliuawa na maafisa wa polisi kwa kufyatuliwa risasi baada ya kufanya hujuma hiyo.

Roula Allouch, Mwenyekiti wa bodi ya taifa ya baraza hilo amesema watu wanaotekeleza hujuma za aina hiyo hawatumi ujumbe duniani kwa niaba ya Waislamu na kwamba mamilioni ya Waislamu nchini Marekani na mabilioni yao kote duniani wanalaani ukatili wa namna hii.

Naye Jennifer Nimer, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria wa baraza hilo katika jimbo la Ohio amesema, na hapa tunamnukuu: "Tunalaani vikali kitendo hicho kisicho cha utu".