Maelfu waandamana Pakistan kulaani mauaji ya Waislamu wa Rohingya
Maelfu ya wananchi wa Pakistan wameandamana kulaani vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.
Maandamano hayo yaliyofanyika jana mjini Karachi Pakistan yamelaani vikali vitendo vya kinyama vinavyofanywa na mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Wakiwa wamebeba mabango na maberamu, waandamanaji hao wametoa mwito wa kuheshimiwa haki za Waislamu hao. Aidha waandamanaji hao walipiga nara dhidi ya serikali ya Myanmar wakitaka kukomeshwa mara moja mauaji hayo na kuheshimiwa haki za Waislamu hao.
Jimbo la Rakhine la Myanmar lina zaidi ya Waislamu milioni moja na maelfu miongoni mwao wameuawa na malaki ya wengine kulazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulio yanayoendelea kufanywa na mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.
Siku chache zilizopita mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zilichomwa moto magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kuendelea ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.
Kuuliwa ovyo jamii hiyo na upuuzaji unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu hao, yote hayo yameufanya Umoja wa Mataifa uwatangaze Waislamu wa Rohingya kuwa ni jamii ya wachache iliyodhulumika zaidi duniani.
Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka na baadhi ya mirengo ndani ya jeshi huko Myanmar wamekuwa wakitekeleza siasa za kuchoma maeneo ya Waislamu lengo likiwa ni kuwafukuza majumbani mwao na kupora ardhi za Waislamu hao. Jambo hilo limewafanya Waislamu wa Rohingya zaidi ya 150,000 kuishi kwa taabu na mashaka katika kambi za wakimbizi huko Myanmar na katika nchi nyingine jirani.