Ban Ki-moon apuuza Palestina katika siku zake za mwisho
Wakati zikiwa zimebakia wiki mbili tu hadi kung'atuka madarakani kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amethibitisha tena kwamba, jumuiya hiyo ya kimataifa imeshindwa kuwa na nafasi na mchango muhimu katika mgogoro wa Palestina.
Miongoni mwa sifa muhimu unazopaswa kuwa nazo Umoja wa Mataifa ni kulinda msingi wa kutopendelea upande wowote na kutekeleza uadilifu katika migogoro ya kimataifa. Hata hivyo inasikitisha kuwa, makati wote viongozi wa umoja huo hawakuwa na sifa hiyo. Bila ya kuashiria jinai zinazoendelea kufanywa na Isarel dhidi ya watu wa Palestina na kushindwa Umoja wa Mataifa kushughulikia uhalifu na jinai hizo, Ban Ki-moon amesema: Hatupasi kuwa na taasubi na misimamo mikali dhidi ya Israel katika Umoja wa Mataifa. Amedai kuwa, katika miongo kadhaa iliyopita kumetolewa maazimio mengi kupita kiasi na vilevile ripoti nyingi dhidi ya Israel ambazo badala ya kusaidia kukomesha mgogoro wa Palestina, vimekuwa sababu ya kufeli na kushindwa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake.
Utawala bandia wa Israel uliundwa katika ardhi za Palestina miaka mitatu tu baada ya kuasisiwa Umoja wa Mataifa hapo mwaka 1945 kwa msaada na himaya ya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo mgogoro wa Israel na Palestina una umri unaokaribiana sana na ule wa Umoja wa Mataifa na hivyo matamshi ya Ban Ki-moon kuhusu mgogoro huo yanaakisi kushindwa na kufeli kwa umoja huo. Sababu kuu ya kushindwa na kufeli huko ni kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijachukua hatua madhubuti za kutekeleza majukumu yake ipasavyo kuhusu mgogoro wa Palestina.
Katika kipindi chote cha uongozi wa muongo mmoja wa Ban Ki-moon, Umoja wa Mataifa ulipasisha mazimio 223 dhidi ya utawala ghasibu wa Israel lakini karibu maazimio yote hayo hayakuwa na dhamana ya utekelezaji wake na yamepuuzwa na Israel. Kinyume kabisa na madai yaliyotolewa na Bai Ki-moon, Umoja wa Mataifa haukufeli katika mgogoro wa Palestina kutokana na kupasisha maazimio mengi, bali ni kutokana na siasa zinazotawala Baraza la Usalama la umoja huo na kuwepo kura ya veto. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maazmio kadhaa yaliyojadiliwa katika Baraza la Usalama yalikwamishwa na kura ya veto ya nchi kama Marekani, Ufaransa na Uingereza licha ya viongozi wa nchi hizo kukosoa kwa maneno matupu uhalifu na jinai zinazofanywa na Wazayuni wa Israel huko Palestina.
Katika hotuba yake, Ban Ki-moon amekosa kwa mbali uvamizi wa Israel huko Palestina lakini inasikitisha kuona kuwa, katika siku hizi za mwishoni mwa uongozi wake katika Umoja wa Mataifa hakusema ni kwa nini umoja huo umeshindwa kusitisha jinai na uvamizi wa Israel. Pamoja na hayo tunapaswa kusema kwamba, ukiachilia mbali Baraza la Usalama, baadhi ya taasisi za Umoja wa Mataifa kama Unicef zimekuwa na mafanikio ya kiasi fulani katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa msingi huo inaeleweka kuwa Baraza la Usalama limeshindwa kutekeleza majukumu yake hususan kuhusu mgogoro wa Palestina kutokana na sababu za kisiasa na vita vya kimaslahi kati ya madola makubwa hususan yale yenye haki ya kutumia kura ya veto. Hali hiyo pia inaonekana katika utendaji wa Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama kuhusu masuala ya Yemen, Iraq, na Syria.