EU yasisitiza tena kutekelezwa kikamilifu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23635-eu_yasisitiza_tena_kutekelezwa_kikamilifu_jcpoa
Umoja wa Ulaya umetilia mkazo kutekelezwa kikamilifu Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kufungamana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya kundi la 5+1 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2017 11:07 UTC
  • EU yasisitiza tena kutekelezwa kikamilifu JCPOA

Umoja wa Ulaya umetilia mkazo kutekelezwa kikamilifu Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kufungamana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya kundi la 5+1 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema leo kabla ya kuanza kikao cha kwanza cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya katika mwaka mpya wa miladia kuwa, leo ni maadhimisho ya kwanza tangu kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na kwamba kutekelezwa makubaliano hayo kunajumuisha azma thabiti ya jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kutekelezwa kikamilifu ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Kikao cha kwanza cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la 5+1 na Iran baada ya kuanza kutekelezwa JCPOA 

Bi Mogherini ameongeza kuwa baada ya kupita mwaka mmoja wameshuhudia taathira muhimu za makubaliano hayo katika uhusiano kati ya Iran na Umoja wa Ulaya; ambazo ni pamoja na kuongezeka biashara na uhusiano wa kiuchumi kati ya pande mbili. Kwa msingi huo Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kufanya juhudi ili kuheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo yenye umuhimu mkubwa. Bi Federica Mogherini aidha ameeleza kuwa matukio ya Syria na amani ya eneo la Mashariki ya Kati ni kadhia ambazo zitajadiliwa mahsusi katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya.