Iran: Nchi za Kiislamu zizuie Waislamu kudhulumiwa duniani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitaka nchi za Kiislamu zisikubali wala kuvumilia kuona Waislamu wakikandamizwa na kudhulumiwa duniani.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyed Abbas Araqchi mpema leo Alhamisi alipohutubu katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC huko Kuala Lumpur nchini Malyasia ambacho kimeitishwa kujadili hali ya Waislamu wa kabila la Rohingya wa Myanmar ambao wanaangamizwa kwa umati na kudhulumiwa.
Araqchi amelaani vikali mauaji ya Waislamu wa Myanmar na kusema ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kufungamana kikamilifu na Waislamu hao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema serikali ya Myanmar inapaswa kudhibiti hali ya mambo na kuhakikisha kuwa Waislamu nchini humo wanaishi maisha yasiyo na bugudha na kuwazuia Mabudha wa nchi hiyo kuwahujumu Waislamu.
Aidha amekumbusha kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ilianzishwa kwa ajili ya kushughulikia kadhia ya mji wa Quds Palestina na kusisitiza kuwa nchi za Kiislamu katika kikao hicho cha Kuala Lumpur zinapawa kutangaza uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina na Quds Tukufu.
Kikao hicho cha wataalamu wa OIC ni utangulizi wa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wananchama ambao watakutana leo Alasiri.
Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wamekuwa wakishambuliwa na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada tokea mwaka 2012 huku vikosi vya usalama navyo vikiwashambulia mara kwa mara. Kutokana na hujuma hizo maelfu ya Waislamu wameuawa na malaki ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi. Serikali ya Myanmar pia imewanyima uraia Waislamu hao na kudai kuwa eti ni wakimbizi walio nchini humo kinyume cha sheria.