Kupelekwa Waislamu wa Myanmar katika kisiwa cha Bangladesh
Serikali ya Bangladesh imesisitiza kutekeleza mpango wa kuwapatia makazi wakimbizi wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya katika kisiwa cha Tangarchar katika Ghuba ya Bengal.
Serikali ya Bangladesh imeunda kamati kadhaa za kusimamia zoezi la utambuzi wa utambulisho wa Waislamu wa Rohingya. Kamati hizo zitaandaa orodha ya wahajiri ambao wanatazamiwa kupelekwa kwa muda katika kisiwa cha Tangarchar katika Ghuba ya Bengal. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, Waislamu wa Rohingya 65,000 ambao wamekimbia mchafuko ya hivi karibuni huko Myanmar, hivi sasa wanaishi kambini huko Bangladesh. Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar wanajaribu kuikimbia nchi hiyo ili kuepuka ghasia na mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo dhidi yao kupitia Ghuba ya Bengal ili kuingia Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia. Aghalabu ya raia hao hukumbwa na matatizo mbalimbali wakiwa baharini kama kutekwa nyara na magenge ya magendo ya binadamu katika safari zao za kuikimbia nchi yao huku wakiwa wamepanda boti zilizojaa kupita kiasi na zisizo na usalama wa kutosha.
Hatua ya kuwahamishia wakimbizi Waislamu wa Myanmar nchini Bangladesh huku vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya jamii hiyo vikiendelea huko Myanmar; inaweza kuongeza idadi ya wakimbizi hao wanaokimbia nchi yao na wakati huohuo kuhatarisha zaidi maisha yao huko Myanmar. Serikali ya Myanmar imeahidi kutazama upya mienendo yake katika kuamiliana na Waislamu wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine nchini humo na kuandaa uwanja wa kuwapatia misaada ya kibinadamu raia hao, baada ya kushinikizwa kieneo na kimataifa kufuatia kufanyika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu (OIC) na kufuatia maombi ya Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) na Umoja wa Mataifa katika uwanja huo. Pamoja na hayo yote, hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa inayothibitisha kutekelezwa ahadi hizo. Suala la kupelekwa katika kisiwa cha Tangarchar huko Bangladesh wakimbizi Waislamu wa Myanmar limezua wasiwasi huu kuwa mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza utaenea katika kambi za kuwahifadhi wakimbizi hao na hata kusababisha maafa ya kibinadamu kutokana na hali isiyoridhisha ya kambi hizo kwa kuzingatia kuwa kisiwa hicho hakina suhula zozote za msingi za kuendeshea maisha na pia kuwepo ugumu wa kufika kisiwani hapo taasisi za kimataifa za misaada ya kibinadamu. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Bangladesh yenyewe inakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha huku ikiwa katika orodha ya nchi maskini, haiwezi kuwadhaminia Waislamu wa Myanmar mahitaji yao. Katika mazingira hayo, jamii ya kimataifa zikiwemo taasisi za kimataifa zinapasa kuishinikiza serikali ya Myanmar ili kuzuia miamala ya kikatili na hujuma za jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa mkoa wa Rakhine na wakati huo huo kuzuia pia kuendelea na kuongezeka wimbi la wakimbizi hao. Kutoroka Myanmar jamii ya Rohingya kwa kutumia usafiri wa boti ili kukwepa mashambulizi na jinai za jeshi na Mabudha wa nchi hiyo wenye misimamo mikali, kunaweza kuwa hatari kwao wenyewe; na vile vile kuzisababishia nchi jirani na Myanmar wimbi la makumi au mamia ya wakimbizi.