Italia kuzisaidia kifedha nchi za Kiafrika ili ziwazuie wahajiri wasielekee Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24573-italia_kuzisaidia_kifedha_nchi_za_kiafrika_ili_ziwazuie_wahajiri_wasielekee_ulaya
Italia imeanzisha mfuko wa fedha wa kuzisaidia nchi za Kiafrika ziimarishe zaidi mipaka yao ili kujaribu kuepusha wahajiri kusafiri kwa kutumia boti dhaifu na hatarishi za mipira kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 02, 2017 02:52 UTC
  • Italia kuzisaidia kifedha nchi za Kiafrika ili ziwazuie wahajiri wasielekee Ulaya

Italia imeanzisha mfuko wa fedha wa kuzisaidia nchi za Kiafrika ziimarishe zaidi mipaka yao ili kujaribu kuepusha wahajiri kusafiri kwa kutumia boti dhaifu na hatarishi za mipira kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Angelino Alfano alitangaza uamuzi huo wa kutoa msaada wa yuro milioni 200 jana Jumatano, siku mbili kabla viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana nchini Malta kujadili mpango wao wa kuwazuia wahajiri kutoka Afrika kuingia barani Ulaya.

Wahajiri 181,000 waliwasili nchini Italia mwaka jana kupitia bahari ya Mediterania, akthari yao wakiwa wameondokea nchini Libya ambako watu wanaowasafirisha kimagendo wahajiri hao wanaendesha shughuli zao pasina kufatiliwa kisheria. Mashirika ya misaada yanakadiria watu zaidi ya 5,000 walifariki dunia mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya.

Wakimbizi kutoka waliofika salama Ulaya

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, kwa sasa Libya, Tunisia na Nigeria ndio washirika wa "kistratijia" wa kupatiwa msaada huo wa pesa lakini Nigeria, Senegal, Misri na Ethiopia nazo pia zinaweza kuwa washirika wa mpango huo katika siku za usoni.

Italia imekosoa mara kadhaa msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na mgogoro wa wahajiri, hasa kwa kushindwa kukubaliana nchi 28 wanachama wa umoja huo juu ya namna ya kugawana wakimbizi na wahajiri wanaokimbilia kwenye nchi hizo…/