Mwandishi habari Mmarekani awaomba radhi Waislamu kutokana na ubaguzi wa Trump
Mwandishi habari maarufu nchini Marekani amewaomba radhi Waislamu wote duniani na kusema: "Wamarekani wanapaswa kusimama kidete dhidi ya watu wenye misimamo mikali."
Nicholas Kristof mwandishi na mwanahabari maarufu Marekani katika makala aliyoandika katika gazeti la New York Times, ameashiria amri ya Rais Donald Trump kuwapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani na kusema amri hiyo inawadhalilisha Wamarekani.
Kristof amesema Trump si muwakilishi wa Wamarekani wote na kuongeza kuwa, Wamarekani wanapaswa kusimama kidete na kupambana na watu wenye misimamo mikali ya kibaguzi na chuki dhidi ya raia wa kigeni. Amesema maamuzi ya Trump yanaimarisha kundi la kigaidi la ISIS na kuhatarisha maisha ya Wamarekani.
Katika makala yake , Kristof ametoa mfano wa mkimbizi msomali Ahmed Ahmed ambaye alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya na kuingia Marekani akiwa na umri wa mwaka moja. Amesema kijana huyo Mwislamu amepata tunzo kama mwanafunzi bora zaidi wa Chuo Kikuu cha Cornell na kuongeza kuwa, watu kama hawa si tishio kwa Marekani.
Kristo ni kati ya waandishi mashuhuri wa Marekani na amepata zawadi mbili za Tunzo Pulitzer ambayo ni tunzo yenye itibari zaidi kwa waandishi habari Marekani.