Makamu wa Rais wa Venezuela: US imeniwekea vikwazo kwa kupinga ubeberu
(last modified Wed, 15 Feb 2017 01:33:27 GMT )
Feb 15, 2017 01:33 UTC
  • Makamu wa Rais wa Venezuela: US imeniwekea vikwazo kwa kupinga ubeberu

Makamu wa Rais wa Venezuela, Tareck El Aissami amekosoa vikali hatua ya Marekani kumuwekea vikwazo eti kwa madai ya kuhusika na ulanguzi wa mihadarati.

El Aissami ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Vikwazo hivi visivyo na thamani na maana vya Marekani dhidi yangu, vimetokana na msimamo wangu wa kuunga mkono mapinduzi dhidi ya madola ya kibeberu."

Radiamali hiyo ni jibu kwa hatua ya Wizara ya Fedha ya Marekani kutangaza vikwazo dhidi ya Makamu wa Rais wa Venezuela na mpambe wake, Samark Jose Lopez Bello, sambamba na kufunga akaunti zao za benki eti kwa kuhusika na magendo ya kutuma mashehena ya mihadarati nchini Marekani.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela (Kulia) na Makamu wake Tareck El Aissami 

Siku ya Jumatatu, mfanyabiashara mashuhuri wa Venezuela Jose Lopez Bello alilaani vikwazo hivyo vya Marekani dhidi yake na Makamu wa Rais wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, huu ni mwendelezo wa sera za uhasama za Washington dhidi ya Caracas. 

Uhusiano wa kidiplomasia wa Venezuela na Marekani uliingia doa mwaka 1999 baada ya hayati Hugo Chavez kuwa rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Nchi mbili hizo hazina mabalozi wa kuziwakilisha katika miji mikuu yao tangu mwaka 2010, ambapo mwezi Machi mwaka jana, Venezuela ilimuita nyumbani mwanadiplomasia wake wa ngazi za juu nchini Marekani kulalamikia hatua ya Washington ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa wakuu wa nchi hiyo. 

 

Tags