Sherehe ya Nowruz yafanyika katika Umoja wa Mataifa
Sherehe ya kuadhimisha sikukuu ya Nowruz imefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa umoja huo.
Ghulam-Ali Khoshroo, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alihutubia sherehe hiyo Jumanne ya jana na kusema utamaduni tajiri wa Nowruz umekuwepo katika kipindi kirefu cha historia na hauwezi kuzuiwa kwa amri yoyote.
Bw. Khoshroo ametoa kauli hiyo akikosoa amri tata ya Rais Donald Trump kuwazuia wasafiri kutoka nchi sita za Kiislamu ambazo ni Iran, Syria, Sudan, Somalia, Libya na Yemen kuingia Marekani.
Aidha amesema kufanyika sherehe za Nowruz katika Umoja wa Mataifa kuna lengo la kuhimiza umoja wa wanadamu na kuongeza kuwa, hivi sasa thamani za kimsingi za mwanadamu zinakabiliwa na tishio. Amezitaja thamani hizo kuwa kama vile wingi wa tamaduni, amani, maelewano, ujirani mwema na kulinda mazingira na kuongeza kuwa, kuna haja zaidi ya wakati wowote mwingine kwa wanadamu kuenzi sikukuu ya Nowruz.

Akihutubu katika sherehe hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema: "Nowruz ni mwanzo mpya, mwaka mpya na fursa ya kuwa pamoja na familia, jamaa na marafiki na kwa msingi huo familia ya Umoja wa Mataifa inasherehekea Nowruz kwa sababu Nowruz ina umuhimu kwa walimwengu wote." Guterres amesema, "Nowruz ni wakati wa kujifunza kuhusu wanadamu wengine na ni fursa ya kutangaza upya kufungamana na amani, urafiki, haki za binadamu na hadhi ya ubinadamu."

Ikumbukwe kuwa Mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza na kuisajili Nowruz, siku ya kwanza ya mwaka wa Hijria Shamsia, kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nairuzi.

Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, siku kuu ya Nowruz hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa wa urafiki baina ya watu wa jamii mbalimbali.