Mataa yazimwa kwa saa moja duniani kulinda mazingira
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26892-mataa_yazimwa_kwa_saa_moja_duniani_kulinda_mazingira
Miji ya nchi 170 duniani, ikiwemo Iran imeshiriki kwenye zoezi la kuzima taa kwa muda wa saa moja jioni ya tarehe 25 Machi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 26, 2017 13:52 UTC
  • Mataa yazimwa kwa saa moja duniani kulinda mazingira

Miji ya nchi 170 duniani, ikiwemo Iran imeshiriki kwenye zoezi la kuzima taa kwa muda wa saa moja jioni ya tarehe 25 Machi.

Zoezi hilo lilianzishwa mwaka 2007 kwa lengo la kuwahamasisha walimwengu watumie mbinu mbalimbali za kupunguza utoaji wa hewa zinazoweza kusababisha kupanda kwa joto duniani, kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira.

Ikiwa ni mara ya kumi, Jumamosi jioni, watu kila mahali walishiriki katika "saa moja ya kujali mazingira ulimwenguni" kama ishara ya kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Katika ujumbe wake kuhusu tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuhatarisha maisha na vipato duniani kote. Ameongeza kuwa, mwaka jana ulikuwa tena mwaka uliovunja rekodi ya juu zaidi ya joto. Aidha amesisitiza kuwa Mkataba wa Paris unatupa fursa ya kipekee ya kuzuia kupanda kwa kiwango cha kimataifa cha joto, kukuza nishati safi kwa wote na kujenga mustakabali endelevu.

Mnara wa Azadi pamoja na ule wa Milad jijini Tehran ilizimwa taa kwa mnasaba wa 'saa moja ya kujali mazingira duniani'

Vile vile ametoa wito kwa serikali na sekta binafsi kwamba ni lazima zifanya juhudi kubwa zaidi kama ambavyo pia amewataka watu binafsi nao wafuate mkondo huo. Amesema jukumu la kuijenga kesho iliyo endelevu, ni la kila mmoja wetu leo hii.

Kwa mnasaba huo maeneo mashuhuri kama vile Mnara wa Milad na Medani ya Azadi mjini Tehran ilizimwa taa kama njia ya Iran ya kujiunga na mataifa mengine duniani kulinda mazingira.