Iran, Russia na Syria zazungumzia mashambulizi ya US dhidi ya Damascus
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27662-iran_russia_na_syria_zazungumzia_mashambulizi_ya_us_dhidi_ya_damascus
Mawaziri wa ulinzi wa Iran, Russia na Syria wamefanya mazungumzo ya simu kuhusu mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya kituo cha kijeshi cha Syria, huku pande tatu hizo zikisisitizia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wao katika vita dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2017 03:15 UTC
  • Iran, Russia na Syria zazungumzia mashambulizi ya US dhidi ya Damascus

Mawaziri wa ulinzi wa Iran, Russia na Syria wamefanya mazungumzo ya simu kuhusu mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya kituo cha kijeshi cha Syria, huku pande tatu hizo zikisisitizia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wao katika vita dhidi ya ugaidi.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerli Hussein Dehqan ameitaja hatua hiyo ya Marekani kama uvamizi wa wazi wa uhuru wa kujitawala Syria na ni kitendo kinachokiuka sheria na hati zote za kimataifa.

Dehqan ameongeza kuwa, Marekani ilitekeleza hujuma hiyo ili kuyapa motisha na kuyashajiisha magenge ya kigaidi nchini Syria, ambayo yalikuwa yanaelekea kusambaratika kikamilifu.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema serikali yake itatumia uwezo wake wa kijeshi sambamba na ushawishi wake wa kisiasa kuyatokomeza makundi ya kigaidi nchini Syria pamoja na wafadhili na waungaji mkono wao.

Mawaziri wa Ulinzi wa Iran (kulia) na Russia

Katika mazungumzo ya simu na Brigedia Jenerali Dehqan, Fahd Jassem al-Freij, Waziri wa Ulinzi wa Syria amesema taifa hilo halibabaishwi na hatua kama hizo za Marekani na kusisitiza kuwa, chokochoko za aina hiyo hazina athari yoyote kwa juhudi zao za kuyaangamiza magenge ya kigaidi nchini.

Wakati huohuo, Mawaziri wa ulinzi wa Iran, Russia na Syria wametoa wito wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza mashambulizi ya silaha za kemikali katika mji wa Khan Shaykhun mkoani Idlib, ambapo makumi ya watu waliuawa. Marekani ilitumia kisingizio hicho bandia dhidi ya serikali ya Damascus kuishambulia Syria.