Waislamu wazidi kunyanyaswa Marekani, msichana avuliwa hijabu hadharani
Unyanyasaji dhidi ya Waislamu unazidi kuongezeka nchini Marekani tangu Donald Trump, rais mwenye chuki na wageni hususan Waislamu alipoingia madarakani nchini humo. Tukio la karibuni kabisa ni kitendo cha mwanamme mmoja mwenye chuki za kidini aliyemvua hijabu hadharani msichana wa Kiislamu, kaskazini mwa mji wa Atlanta, huko Marekani.
Shirika la habari la Associated Press limetangaza kuwa, msichana mmoja Muislamu mwenye umri wa miaka 14 amevuliwa vazi la staha ya Kiislamu la hijabu, kaskazini mwa mji wa Atlanta, wakati alipokuwa kwenye duka moja kubwa akinunua vitu. Mtu huyo alimvamia na kumshambulia msichana huyo bila ya sababu yoyote na kumvua hijabu huku akimwita gaidi.
Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu limeweka zawadi ya dola elfu moja kwa mtu yeyote atakayepelekea kukamatwa mtu huyo mwenye chuki za kidini.
Edward Ahmad Michel, mkurugenzi mtendaji wa baraza hilo katika jimbo la Georgia amesema kuwa, shambulio hilo limeitisha na kuitia hofu kubwa familia ya msichana huyo.
Vitendo vya unyanyasaji wa Waislamu ikiwa ni pamoja na kushambuliwa Waislamu hao na kuvunjiwa heshima maeneo yao vimeongezeka sana nchini Marekani tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump, mwenye chuki na wageni, hasa Waislamu.