Lavrov: Russia, Iran, Hizbullah zitaendelea kuiunga mkono Syria kupambana na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28142-lavrov_russia_iran_hizbullah_zitaendelea_kuiunga_mkono_syria_kupambana_na_magaidi
Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametilia mkazo wajibu wa kubadilishwa misimamo ya nchi za Magharibi katika suala zima la kupambana na magenge ya kigaidi nchini Syria na kusema kuwa, Moscow, Tehran na Hizbullah zinaiunga mkono Damascus katika vita dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2017 03:22 UTC
  • Lavrov: Russia, Iran, Hizbullah zitaendelea kuiunga mkono Syria kupambana na magaidi

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametilia mkazo wajibu wa kubadilishwa misimamo ya nchi za Magharibi katika suala zima la kupambana na magenge ya kigaidi nchini Syria na kusema kuwa, Moscow, Tehran na Hizbullah zinaiunga mkono Damascus katika vita dhidi ya ugaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imenukuu matamshi ya Lavrov akisema kuwa, jeshi la Syria kwa msaada wa kikosi cha anga za juu cha Russia na ushauri wa kijeshi wa Iran pamoja na wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon ambao wote wanafanya hivyo baada ya kuombwa na serikali halali ya Syria, limepata mafaniko makubwa katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi.

Amesema muungano unaoongozwa na Marekani kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Magharibi na Uturuki umethibitisha kuwa hauna lengo la kupambana na magenge ya kigaidi kwani kama mashambulizi ya muungano huo yangelielekezwa kweli kwenye vita dhidi ya magaidi wa Daesh na Jabhatunnusra nchini Syria, matokeo ya mashambulizi hayo yangelikuwa mazuri na kusingelikuwa na magenge ya kigaidi na kitakfiri huko Syria.

Mfumo wa kujilinda na makombora wa S400 wa Russia. Uungaji mkono wa Russia, Iran na Hizbullah umeimarisha nguvu za Syria

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, nchi yake inapigania kuimarishwa makubaliano ya kusimamisha vita na kuendelea mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria, tabáni bila ya kushirikishwa na magenge ya kigaidi kama vile Daesh na Jabhatunnusra.

Ikumbukwe kuwa Iran, Russia na Uturuki ndio wasimamiaji wakuu wa mazungumzo ya amani ya Syria ya Astana, mji mkuu wa Kazakhstan na hadi hivi sasa kumeshafanyika duru tatu za mazungumzo hayo na kushirikisha pia serikali ya Syria, makundi ya wapinzani na Umoja wa Mataifa.