Russia: Marekani iache unafiki na undumakuwili
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameitaja Marekani pamoja na waitifaki wake wa Magharibi kuwa ni wanafiki kwa kukataa kulaani hujuma za hivi karibuni dhidi ya ubalozi wa Russia nchini Ukraine.
Katika mahojiano na Kanali ya Televisheni ya Ren TV ya Russia, Sergei Lavrov ameeleza kughadhabishwa kwake na kimya cha Wamagharibi juu ya kushambuliwa ubalozi wa nchi yakje nchini Ukraine na kutaja hatua hiyo kuwa ya kinafiki na ya undumakuwili.
Jumatano iliyopita, waandamanaji waliokuwa na ghadhabu waliushambulia ubalozi wa Russia katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, ambapo genge la wahuni lilirusha mawe, vidonge vya kutoa machozi, mayai na chupa zenye kemikali aina ya iodine kwenye jengo la ubalozi huo.
Hii sio mara ya kwanza kwa uvamizi wa namna hii kutokea dhidi ya ubalozi wa Russia mjini Kiev. Jumapili iliyopita, hujuma sawa na hiyo ilitokea katika ubalozi huo ambapo makundi ya watu yaliteketeza magari ya wanadiplomasia wa Russia usiku kucha, kuchana bendera ya nchi hiyo na kurusha mabomu ya moshi katika jengo hilo.
Lavrov amesema licha ya serikali ya Moscow kuwa na uwepesi wa kulaani shambulizi la aina yoyote dhidi ya balozi mbalimbali, lakini wameshangazwa na namna Marekani na waitifaki wake wa Magharibi mpaka sasa hawajatoa kauli yoyote kuhusu hujuma hizo mbili dhidi ya ubalozi wa Russia mjini Kiev nchini Ukraine.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Aprili mwaka jana, jeshi la Marekani lilituma askari 300 nchini Ukraine kwa madai ya kutoa mafunzo kwa Kikosi cha Ulinzi wa Taifa cha nchi hiyo (NGU), ambacho kinapigana na vikosi vya waitifaki wa Russia mashariki mwa Ukraine.