Ufilipino: Miripuko ya mjini Manila, ilimlenga imamu wa Kishia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28790-ufilipino_miripuko_ya_mjini_manila_ilimlenga_imamu_wa_kishia
Kamanda wa polisi nchini Ufilipino amesema kuwa, miripuko miwili iliyotokea mjini Manila, mji mkuu wa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu wawili, ilikuwa imemlenga imamu wa jamaa wa Kishia mjini hapo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 07, 2017 23:34 UTC
  • Ufilipino: Miripuko ya mjini Manila, ilimlenga imamu wa Kishia

Kamanda wa polisi nchini Ufilipino amesema kuwa, miripuko miwili iliyotokea mjini Manila, mji mkuu wa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu wawili, ilikuwa imemlenga imamu wa jamaa wa Kishia mjini hapo.

Oscar Albayalde, amesema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba hujuma hiyo ilikuwa imemlenga Sheikh Nasser Abinal. Katika shambulizi hilo watu wengine sita walijeruhiwa. Bomu la kwanza lilikuwa limefungwa katika mfuko ambao kabla ya kuripuka, alipewa Sheikh Abinal.

Eneo kulipojiri shambulizi hilo 

Polisi wameanzisha uchunguzi kwa ajili ya kufahamu wahusika wa shambulizi hilo. Hata hivyo kwa mujibu wa Oscar Albayalde, miripuko hiyo haina mahusiano na makundi yanayofahamika ya ugaidi, kwa kuwa hadi sasa hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuwepo mkono wa kundi lolote la kigaidi ndani na nje ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo tayari kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na hujuma hiyo. Daesh imesema kuwa katika hujuma hiyo Waislamu watano wa Shia wameuawa. 

Sheikh Nasser Abinal kulia

Akijibu madai ya kundi hilo, Albayalde amesema kuwa, ni kawaida ya genge hilo la (ISIS) kutangaza kuhusika na hujuma katika nchi mbalimbali hata kama halijahusika. Sheikh Nasser Abinal amekuwa akiendesha harakati za kulingania umoja baina ya Waislamu wa Suni na Shia nchini Ufilipino.