Mahakama yaagiza kucharazwa viboko mahanithi huko nchini Indonesia
Mahakama ya Kiislamu nchini Indonesia imetoa hukumu ya kucharazwa viboko 85 hadharani, mahanithi wawili waliopatikana na hatia ya kufanya liwati na kujihusisha na uhusiano wa jinsia moja.
Ikitoa hukumu hiyo jana Jumatano, mahakama hiyo iliyopo katika mkoa wa kihafidhina wa Aceh imeagiza vijana hao wenye umri wa miaka 20 na 23 watandikwe viboko 85 kila mmoja, kwa kujihusisha na uchafu huo.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo inayotoa hukumu kwa mujbu wa sheria za Kiislamu aliyetambuliwa kwa jina moja la Gulmaini amesema hukumu hiyo itatekelezwa wiki ijayo, kabla ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Aceh ndio mkoa wa pekee Indonesia, nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu, unaofuata kikamilifu na kutekeleza sharia za Kiislamu.
Mapema mwezi huu, Basuki Tjahaja Purnama, Gavana anayeondoka wa Jakarta, mji mkuu wa Indonesia alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kuuvunjia heshima na kuudhalilisha Uislamu.
Purnama ambaye ni Mkristo alipoteza kiti cha ugavana katika duru ya pili ya uchaguzi mwezi Aprili, ambapo alishindwa na Anies Baswedan, mwanasiasa Mwislamu.