Jun 17, 2017 04:34 UTC
  • Waingereza waitaka serikali kutoa sababu ya kuteketea jengo kongwe, Waislamu wasifiwa

Kufuatia tukio la kuteketea moto jengo kongwe mjini London, wakazi wa mji huo wameitaka serikali ya Uingereza kutaja chanzo cha moto huo ambao umesababisha hasara kubwa ya mali na roho.

Wakazi wa mji huo ambao wameonyesha hasira kali kutokana na kupotelewa na ndugu na jamaa zao katika tukio hilo wamewataka viongozi wa nchi hiyo kutoa majibu kamili haraka iwezekanavyo.

Jengo hilo kongwe la makazi likiteketea moto

Hii ni katika hali ambayo idara ya zimamoto mjini London imetangaza kwamba, idadi ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo bado haijajulikana. Kwa mujibu wa idara hiyo, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha katika mkasa huo. Baada ya wakazi wa mji wa London kumuona Sadiq Khan, ambaye ni meya wa mji huo katika eneo la tukio, walimwambia kuwa ni lazima serikali itoe maelezo ya kutosha kuhusiana na suala hilo. Vyombo vya habari nchini humo vimetangaza kuwa, idadi ya wahanga na watu waliopotea katika tukio hilo ni 65 pekee. Moto huo ulitokea siku ya Jumatano wakati wakazi wengi wa jengo hilo walikuwa bado wamelala. Kufuatia hali hiyo, asasi kadhaa za Kiislamu mjini London zimeshiriki kwa kiasi kikubwa katika kutoa misaada mbalimbali kwa wahanga wa tukio hilo.

Sehemu ya msaada wa Waislamu wa London kwa wahanga wa tukio hilo

Waingereza mbalimbali wametoa shukurani zao kwa Waislamu hao ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa michango na misaada yao kwa wahanga wa tukio hilo wakisema kuwa, suala hilo limeonyesha kuwa dini ya Uislamu ni dini ya upendo na amani.

Tags