Kikao cha kushukuru mchango wa Waislamu chafanyika nchini Brazil
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31448-kikao_cha_kushukuru_mchango_wa_waislamu_chafanyika_nchini_brazil
Kikao cha kuheshimu na kutambua mchango wa jamii ya Waislamu wa Brazil kilifanyika jana katika bunge la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2017 07:50 UTC
  • Kikao cha kushukuru mchango wa Waislamu chafanyika nchini Brazil

Kikao cha kuheshimu na kutambua mchango wa jamii ya Waislamu wa Brazil kilifanyika jana katika bunge la nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, kikao hicho kimeshirikisha wawakilishi wa jamii tofauti wakiwemo pia wajumbe wa Kituo cha Kiislamu cha Brazil, mabalozi na wawakilishi wa ofisi za kibalozi zilizoko nchini humo pamoja na wabunge wa nchi hiyo.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kutambua nafasi na mchango wa Waislamu milioni mbili wa Brazil hususan kutokana na tabia yao nzuri ya usamehevu na kuishi kwa amani na usalama na watu wa jamii nyinginezo katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Waislamu ni watu wanaopenda amani popote walipo

 

Katika kikao hicho cha jana Alkhamisi, wawakilishi wa jamii za Kiislamu walisisitiza kuwa ugaidi hauna uhusiano wowote na mafundisho matukufu ya Kiislamu na kuongeza kwamba, vitendo vya kigaidi ni mgogoro mkubwa ambao unalenga usalama wa dunia nzima na hauna uhusiano na mafundisho ya dini yoyote ile.

Mwishoni mwa kikao hicho kumesisitiziwa wajibu wa kuishi pamoja kwa amani na kusameheana na kuwataka wananchi wote wa Brazil kuzidi kupendana na kuishi kwa kushirikiana.

Waislamu wa Brazil wakipeperusha bendera ya nchi yao