Zarif: Marekani imekiuka mapatano ya nyuklia na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31858
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani imekiuka utekelezaji wa ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya Iran.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jul 17, 2017 03:52 UTC
  • Zarif: Marekani imekiuka mapatano ya nyuklia na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani imekiuka utekelezaji wa ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya Iran.

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye yuko New York Marekani kushiriki katika kikao cha ngazi za juu cha  kisiasa katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumapili katika mahojiano na televisheni ya CNN aliashiria utendaji wa Marekani kuhusu mapatano ya nyuklia na kusema: "Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake katika mapatano ya nyuklia na hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umethibitisha suala hili lakini Marekani haijatekeleza ahadi zake."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha akijibu swali kuhusu uwezekano wa Iran kumiliki silaha za nyuklia hata baada ya mapatano yake ya nyuklia na nchi za 5+1 amesema: "Iran katika mchakato wa kufikiwa mapatano na hata kabla ya hapo ilitangaza wazi kuwa haifuatilii mpango wa silaha za nyuklia na hata IAEA imethibitisha kuwa madai ya kuwepo muelekeo wa kijeshi katika mpango wa nyuklia wa Iran hayana msingi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia pia kuhusu sababu za Iran kuiunga mkono Syria kijeshi na kuongeza kuwa: "Sera za Iran kuhusu Syria, Afghanistan, Iraq na maeneo mengine ya eneo ni kuleta uthabiti; Iran inapinga ugaidi na misimamo mikali na inawasaidia wale ambao wanapambana na ugaidi na misimamo mikali."

Zarif katika mahojiano na CNN

Kuhusu mgogoro wa Yemen Zarif amesema: "Iran inapinga mapigano Yemen na imependekeza mpango wa vipengee vinne nchini Yemen unaojumuisha usitishwaji vita, kufikisha misaada ya kibinadamu, mazungumzo ya Wayemen kwa Wayemen, na kuunda serikali kwa msingi wa matakwa ya Wayemen." Amesema hii ndio njia pekee ya kumaliza vita Yemen na kwamba ukweli ni kuwa mgogoro wa Yemen hauna suluhisho la kijeshi.

Akitoa mtazamo wake kuhusu ripoti ya hivi karibuni ya gazeti la New York Times ambalo lilidai kuwa 'Iran imeeneza satwa yake Iraq', Zarif amesema Iran daima imekuwa ikichukua maamuzi sahihi na iko tayari kuwasaidia watu wa Iraq kinyume cha nchi ambazo zilimuunga mkono Saddam na zinaunga mkono kundi la ISIS na makundi mengine ya kigaidi. Amesema waitifaki wa Marekani ndio wanaounga mkono magaidi wa ISIS, al-Nusra na AL Qaeda kifedha na kiadiolojia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameelezea masikitiko yake kuwa Saudi Arabia inaeneza itikadi inayochochea misimamo mikali duniani.