Venezuela yajibu mapigo baada ya vitisho vya uingiliaji kijeshi wa Trump
(last modified Tue, 15 Aug 2017 07:35:59 GMT )
Aug 15, 2017 07:35 UTC
  • Venezuela yajibu mapigo baada ya vitisho vya uingiliaji kijeshi wa Trump

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameliagiza jeshi la nchi hiyo kufanya luteka ya nchi nzima ikiwa ni radiamali kwa vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani aliyesema kuwa chaguo la kuishambulia kijeshi nchi hiyo lipo mezani.

Maduro aliyasema hayo jana akiwahutubia wananchi waliofanya maandamano katika mji mkuu Caracas kulaani vitisho hivyo vya Marekani dhidi ya taifa hilo.

Amesema mazoezi hayo ya kijeshi yatafanyika juma lijalo Agosti 26 na 27 kwa kuvishirikisha vikosi vyote vya jeshi la nchi hiyo.

Katika maandamano ya jana, Jenerali Vladimir Padrino, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela alisema Marekani imeamua 'kufichua uso wake' na sasa inaonyesha wazi ilivyo na hamu ya kutaka kuishambulia nchi yake.

Wakuu wa jeshi wa Venezuela

Rais wa Venezuela hivi karibuni alifuchua kuwa, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA linashirikiana na Mexico na Colombia katika njama ya kuipindua serikali halali ya Caracas, kwa lengo la kulinda maslahi yao ya mafuta.

Mwezi Februari mwaka huu, siku chache baada ya kuapishwa, Trump alikutana na mke wa Leopoldo López, kiongozi mkuu wa upinzani anayezuiliwa katika jela nchini Venezuela, hatua iliyokoselewa vikali na serikali ya Maduro na kusema kuwa walikutana kupanga mikakati ya kuvuruga umoja na amani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Tags