Mkuu wa Majeshi Myanmar: Hatutasitisha mashambulizi yetu kuwalenga Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34519-mkuu_wa_majeshi_myanmar_hatutasitisha_mashambulizi_yetu_kuwalenga_waislamu_wa_rohingya
Licha ya ukosoaji na kulaaniwa na jamii ya kimataifa mauaji na ukandamizaji unaofanywa na askari wa serikali ya Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha magaidi kuwalenga Waislamu wa jamii ya wachache wa Rohingya, mkuu wa majeshi ya nchi hiyo amesisitiza kuwa jeshi hilo litaendeleza hujuma na mashambulizi hayo dhidi ya jamii hiyo ya Waislamu.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 18, 2017 03:31 UTC
  • Mkuu wa Majeshi Myanmar: Hatutasitisha mashambulizi yetu kuwalenga Waislamu wa Rohingya

Licha ya ukosoaji na kulaaniwa na jamii ya kimataifa mauaji na ukandamizaji unaofanywa na askari wa serikali ya Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha magaidi kuwalenga Waislamu wa jamii ya wachache wa Rohingya, mkuu wa majeshi ya nchi hiyo amesisitiza kuwa jeshi hilo litaendeleza hujuma na mashambulizi hayo dhidi ya jamii hiyo ya Waislamu.

Min Aung Hlaing aliyasema hayo Jumapili ambapo sambamba na kutetea operesheni za jeshi la nchi hiyo katika kuwaua Waislamu wa Rohingya alisema kuwa, operesheni hizo kwa ajili ya kuwaondoa Waislamu hao kutoka nchi hiyo zitaendelea. Hii ni katika hali ambayo chama cha Mrengo wa Kitaifa kwa ajili ya Demokrasia nchini Myanmar ambacho ndio chama tawala, kimetangaza kuungana na jeshi katika kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Rohingya wa nchi hiyo.

Walimwengu wakiendelea kuandamana kulaani mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Myanmar

Sisitizo la chama tawala na jeshi juu ya kuendelezwa mashambulizi na mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, limetolewa katika hali ambayo mauaji na jinai hizo zimekuwa zikilaaniwa vikali na nchi za eneo na jamii ya kimataifa na kutaka kukomeshwa haraka wimbi hilo la jinai. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu, zaidi ya Waislamu elfu sita wa Rohingya wameuawa na Mabudha magaidi kwa kushirikiana na askari wa serikali ya nchi hiyo. Aidha katika mashambulizi hayo ya kinyama, zaidi ya Waislamu wengine elfu nane wamejeruhiwa, huku wengine zaidi ya laki nne wakilazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi hiyo.

Silaha za Wamagharibi na Israel zinatumika katika kuwaua kwa halaiki Waislamu

Serikali ya Myanmar inadai kuwa Waislamu wa Rohingya ni wahamiaji haramu kutoka India na Bangladesh, katika hali ambayo historia zinaonyesha kwamba jamii hiyo ya Waislamu imekuwepo katika mkoa wa Rakhine tangu karne ya 12 Miladia zaidi ya jamii nyingine yoyote ile ya nchi hiyo. Uungaji mkono wa Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Magharibi kwa serikali ya Myanmar, unatajwa kuwa chanzo cha jeuri ya viongozi wa nchi hiyo katika kuendeleza mauaji ya halaiki dhidi ya jamii hiyo ya Waislamu wasio na hatia.