WFP: Jamii ya kimataifa iwatumie misaada Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35105-wfp_jamii_ya_kimataifa_iwatumie_misaada_waislamu_wa_rohingya
Mpango wa Chakula Duniani WFP umeitaka jamii ya kimataifa kufanya hima kunusuru maisha ya mamia ya maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya wanaohitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2017 00:57 UTC
  • WFP: Jamii ya kimataifa iwatumie misaada Waislamu wa Rohingya

Mpango wa Chakula Duniani WFP umeitaka jamii ya kimataifa kufanya hima kunusuru maisha ya mamia ya maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya wanaohitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.

David Beasley, Mkuu wa masuala ya misaada ya chakula wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa amesema wakimbizi wa Rohingya walioko nchini Bagladesh wananyemelewa na mgogoro mkubwa wa hali mbaya ya kibinadamu iwapo hawatapokea misaada ya kibinadamu hususan chakula.

Amesema WFP inahitaji dola milioni 75 za Marekani katika kipindi cha miezi mitano hadi sita ijayo ili kukidhi hitaji la chakula kwa ajili ya wakimbizi hao.

Nembo ya WFP

Afisa huyo wa WFP amesema shirika hilo la UN tayari limesajili zaidi ya wakimbizi laki 4 na elfu 60 wa Rohingya katika kambi za wakimbizi zilizoko katika eneo la Kutupalong karibu na wilaya ya Cox nchini Bangladesh.

Takwimu mpya za Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinasema kuwa idadi ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya imepindukia laki 5.

Hivi karibuni Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliitaka serikali ya Myanmar isitishe mashambulio yake dhidi ya Waislamu magharibi na mwa nchi hiyo na iandae mazingira ya wananchi hao kupatiwa himaya na misaada ya kibinadamu.