Uingereza yajipanga kupigana na Korea ya Kaskazini
Gazeti moja linalochapishwa nchini Uingereza limeashiria kupamba moto mivutano ya maneno kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini na kuandika kuwa Uingereza yenyewe inajiandaa kuhusu uwezekano wa kujiri vita kati yake na Pyongyang.
Gazeti la Daily Telegraph limeandika kuwa Korea ya Kaskazini leo Jumanne inalifanyia majaribio kombora lake jingine la masafa ya mbali na kwamba hatua hiyo huenda ikaipelekea Washington ichukue hatua za kijeshi; na ndio maana viongozi wa Uingereza pia wanajitayarisha kwa ajili ya vita na Korea ya Kaskazini.
Daily Telegraph limekinukuu chombo kimoja cha kuaminika na kuandika kuwa, Uingereza itakuwa sehemu ya muungano wa kimataifa dhidi ya Korea ya Kaskazini iwapo kutatokea vita kati yake na Pyongyang.
Rais Donald Trump wa Marekani Jumamosi iliyopita alituma ujumbe katika ukurasa wake wa twitter akisema kuwa, kuna chaguo moja kuhusu Korea ya Kaskazini ambapo jambo hilo linaashiria hatua ya kijeshi kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Hii ni katika hali ambayo mamia ya wanaharakati wanaopinga vita na makundi ya kiraia mwezi uliopita waliandamana mkabala na ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza mjini London wakimtaka ajiepushe na vita baina ya nchi hiyo na Korea ya Kaskazini.