Watoto wakimbizi wa Rohingya wafanywa watumwa wa ngono
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35823-watoto_wakimbizi_wa_rohingya_wafanywa_watumwa_wa_ngono
Wanaofanya magendo ya binadamu na biashara haramu ya utumwa wa ngono wameanza kuwavizia wanawake na watoto wadogo wa jamii ya Rohingya waliofurika katika kambi za wakimbizi zilizoko katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2017 04:23 UTC
  • Watoto wakimbizi wa Rohingya wafanywa watumwa wa ngono

Wanaofanya magendo ya binadamu na biashara haramu ya utumwa wa ngono wameanza kuwavizia wanawake na watoto wadogo wa jamii ya Rohingya waliofurika katika kambi za wakimbizi zilizoko katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh.

Zia Choudhury, Mkurugenzi Mkuu wa kundi la kibinadamu la CARE nchini Bangladesh amenukuliwa na shirika la habari la ABC News akisema wakimbizi hao Waislamu wa jamii ya Rohingya mbali na kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu, sasa wanakodolewa macho na tishio jipya.

Amesema: "Tumepokea taarifa kuwa kuna makundi fulani ya watu yanawanyemelea wanawake na watoto wadogo katika kambi hizi wakiwahadaa kuwa watawapeleka sehemu salama na kuwapa ajira. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, yumkini wakapelekwa sehemu za kuogofya na kufanyiwa madhila mabaya zaidi kuliko kambini wanakoishi."

Wakati huo huo, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema asilimia 58 ya wakimbizi laki 6 waliokimbilia Bangladesh ndani ya wiki nane zilizopita ni watoto wadogo, ambao wanakabiliwa na hali mbaya sana ya kibinadamu.

Mama na mwanawe wa
Kirohingya wakiwa katika kambi ya wakimbizi Bangladesh

Wiki iliyopita, Idara ya Huduma za Kijamii nchini Bangladesh ilisema watoto karibu 14 elfu wa Rohingya wamekuwa mayatima baada ya kupoteza wazazi wao katika mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii hiyo nchini Myanmar.

Takwimu zinaonesha kuwa, maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuawa na malaki ya wengine wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh kufutia mashambulizi yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar wenye misimamo ya kuchupa mipaka wakishirikiana na jeshi la nchi hiyo tangu Agosti 25 mwaka huu.