Iran yamhukumu kifo jasusi wa Mossad ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35925-iran_yamhukumu_kifo_jasusi_wa_mossad_ya_israel
Mwendesha mashtaka wa Tehran amesema ajenti wa Shirika la Ujasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kuipa Tel Aviv taarifa zilizopelekea kuuawa shahidi wataalamu wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Oct 25, 2017 00:33 UTC
  • Iran yamhukumu kifo jasusi wa Mossad ya Israel

Mwendesha mashtaka wa Tehran amesema ajenti wa Shirika la Ujasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kuipa Tel Aviv taarifa zilizopelekea kuuawa shahidi wataalamu wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Abbas Jafari Dolatabadi aliyasema haya jana Jumanne na kuongeza kuwa, moja ya makosa aliyoyafanya jasusi huyo wa Israel ni kutoa anwani na habari za kibinafsi za wataalamu 30 wa kijeshi na miradi ya nyuklia ya Iran, wakiwemo mashahidi Shahriari na Ali-Mohammadi, kwa maafisa wa MOSSAD.

Amefafanua kuwa, kitendo hicho ndicho kilichopelekea kuviziwa na kuuawa shahidi watalaamu hao wa nyuklia wa Kiirani.

Mwendesha mashtaka wa Tehran ameongeza kuwa, ajenti huyo alikutana na maafisa wanane wa Shirika la Ujasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD na kuwapa taarifa nyeti na za siri kuhusu vituo vya kijeshi vya Iran na shughuli za Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limekuwa likifanya kazi kwa karibu na MOSSAD ya Israel

Vyombo vya usalama vya Iran vilimtia mbaroni Majid Jamali Fashi siku chache baada ya kuuawa shahidi mtaalamu wa nyuklia wa Iran, Ali-Mohammadi, ambaye baadaye alikiri kutekeleza mauaji hayo ya Januari mwaka 2010, chini ya maagizo na maelekezo ya MOSSAD.

Wataalamu wengine wa nyuklia wa Iran waliouawa shahidi na maajenti wa MOSSAD ni pamoja na Majid Shahriari (Novemba 2010), Dariush Rezaei Nejad (Julai 2011), na Mostafa Ahmadi Roshan (Januari 2012).