Israel kuwafukuza kwa nguvu wahajiri Waafrika
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amefikia makubaliano na viongozi wa nchi za Afrika kuhusiana na kuwarejesha kwa nguvu Waafrika wanaoingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.
Makubaliano hayo yalifanyika pambizoni mwa Mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, mwezi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Hayom, katika mazungumzo ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na viongozi hao wa Afrika imekubaliwa kwamba wahajiri wote Waafrika walioingia kinyume cha sheria katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu warejeshwe kwa nguvu katika nchi zao.
Wengi wa wahajiri hao ni kutoka Sudan na Eritrea na wamekuwa wakiingia katika ardhi hizo za Palestina kupitia mpaka wake wa jangwani na Misri.
Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alisema kuwa, eneo la kusini mwa Tel Aviv ambalo liko mikononi mwa wahajiri kutoka Afrika litarejeshwa kwa Mayahudi baada ya kufukuzwa kwa nguvu wahajiri hao.
Katika miaka ya hivi karibuni, makumi ya maelfu ya raia wa nchi za Afrika hususan kutoka Eritrea na Sudan wamekuwa wakiingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel kupitia jangwani ingawa wanapofika huko wanakabiliwa na matatizo mengi kutoka kwa Wazayuni ikiwa ni pamoja na kutimuliwa mara kwa mara katika maeneo wanayokimbilia.