Wananchi wa Indonesia waandamana kuwaunga mkono Wapalestina
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Indonesia wamefanya maandamano Jumapili ya leo kulaani uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.
Wananchi zaidi ya 80 elfu wameshiriki maandamano hayo yaliyoandaliwa na Baraza la Maulamaa wa Kiislamu nchini humo katikati ya mji mkuu Jakarta.
Huku wakipeperusha bendera ya Palestina, waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara zinasosema: Mungu ni Mkubwa! Palestina iachwe huru!
Miongoni mwa walioshiriki maandamano hayo ni Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo, Lukman Hakim Saifuddin na Gavana wa mji mkuu Jakarta.
Tarehe 6 ya mwezi huu wa Disemba, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuitambua rasmi Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kutaka yafanyike maandalizi ya kuuhamishia huko Quds inayokaliwa kwa mabavu ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv. Hatua hiyo ya Trump imekabiliwa na upinzani mkubwa wa walimwengu, viongozi wa nchi na jumuiya za kimataifa.
Mbali na ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu maandamano ya kupinga na kulaani uamuzi huo wa Trump yangali yanaendelea kufanywa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu na hata katika nchi za Magharibi ambazo zimeeleza kutiwa wasiwasi na uamuzi huo.