Mwanastratijia wa rais wa Marekani: Wasaudia wanaiogopa kama kufa Iran
Mwanastratijia wa ngazi ya juu wa zamani wa rais nchini Marekani amesema kuwa, Wasaudia wanaiogopa kama kufa Iran.
Stephen K. Bannon ameyasema hayo wakati alipozungumzia kitabu cha Moto na Ghadhabu 'Fire and Fury' ambacho kinazungumzia mwaka mmoja wa kuingia katika Ikulu ya White House rais wa Marekani Donald Trump na kuongeza kuwa, utawala wa Aal-Saud uko katika ukingo wa shimo la kuangamia.
Katika siku za hivi karibuni kitabu Moto na Ghadhabu kilichoandikwa na Michael Wolff kimepata umashuhuri mkubwa huku kikiendelea kununuliwa na Wamarekani wengi, ingawa kimeibua hasira kali ya Trump. Aidha katika kitabu hicho, Bannon sambamba na kuashiria vita vya Saudia na washirika wake dhidi ya Yemen, ameelezea khofu ya hali ya juu waliyo nayo Aal Saud kwa Iran. Saudia imekuwa ikifanya mashambulizi makubwa ambayo yamesababisha mauaji ya maelfu ya watu kwa kile inachodai kuwa ni kutaka kuisambaratisha harakati ya Answarullah ambayo inazidi kupata nguvu na ushawishi mkubwa nchini Yemen.
Viongozi wa Saudia wanadai kuwa eti harakati hiyo inapata msaada kutoka Iran, madai ambayo wameshindwa kuyatibitisha hadi hivi sasa. Mwandishi huyo wa kitabu cha 'Moto na Ghadhabu' amesema amewafanyia mahojiano watu 200 wakati anajiandaa kuandika kitabu hicho na hatimaye alijikinaisha kwamba, usalama wa akili ya Trump unatia shaka.