Jan 11, 2018 16:20 UTC
  • Mtazamo wa Warussia waliowengi: Marekani ni adui nambari moja wa Russia

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo kimoja cha umma nchini Russia yanaonyesha kuwa akthari ya Warussia wanaamini kuwa Marekani ndiye adui yao nambari moja.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha Levada Centre na kutangazwa siku ya Jumatano umeonyesha kuwa asilimia 68 ya watu waliotoa maoni yao wanaamini kuwa Marekani ingali adui nambari moja wa Russia.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kuhusiana na uchunguzi huo, katika uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo hicho hicho miaka mitano nyuma, asilimia 56 ya Warussia walikuwa wakiitakidi kwamba Marekani ni adui nambari moja wa nchi yao; ndiyo kusema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitano, kiwango cha mtazamo mbaya waliokuwa nao Warussia kwa Marekani kimeongezeka kwa asilimia 12.

Kwa mujibu wa takwimu za uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na kituo cha Levada, asilimia 29 ya waliotoa maoni yao wanahisi kuwa baada ya Marekani, Ukraine ni adui nambari mbili wa nchi yao, huku wasilimia 14 wakiitakidi kwamba Umoja wa Ulaya ni adui nambari tatu wa Russia.

Uchunguzi huo wa maoni ulifanywa mwishoni mwa mwezi uliopita wa Desemba 2017 ambapo watu 1,600 wa marika tofauti kutoka maeneo 137 ya Russia walitakiwa kutoa maoni yao kwa kujaza fomu maalumu ya masuali.../

Tags