Feb 01, 2018 14:07 UTC
  • Ripoti: Waislamu wa Rohingya walimwagiwa asidi usoni kabla ya kuzikwa hai

Makaburi matano mapya ya umati yamegunduliwa katika vijijini vya mkoa wa Rakhine nchini Myanmar, ambapo baadhi ya Waislamu wa Rohingya walimwagiwa tindikali katika nyuso zao kabla ya viwiliwili vyao kufukiwa wakiwa hai.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Associated Press umebainisha kuwa, Waislamu hao wa jamii ya Rohingya walifanyiwa ukatili huo na wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali katika vijiji vya Gu Dar Pyin na Buthidaung mkoani Rakhine.

Huku wakiwa na ushahidi wa picha na kanda za video zilizorekodiwa kwenye simu zao za rununu, manusura zaidi ya 20 wa matukio hayo ya kinyama wamelionyesha shirika hilo la habari namna Waislamu hao hususan wanaume, walivyomwagiwa asidi usoni au vichwa vyao kuharibiwa kikamilifu kwa kufyatuliwa risasi kwa karibu, kabla ya maiti hizo kuzikwa nusu.

Hii ni katika hali ambayo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) hivi karibuni lilisema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Makaburi ya umati mkoani Rakhine

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea Warohingya 655,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh kutafuta hifadhi.

Tags