Rais Rouhani asisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu dhidi ya maadui
(last modified Fri, 16 Feb 2018 13:55:00 GMT )
Feb 16, 2018 13:55 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu dhidi ya maadui

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu kote duniani, mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel na maadui wengine wa Uislamu na Waislamu.

Rais Rouhani ametoa sisitizo hilo hii leo baada ya kuhudhuria Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Makka mjini Hyderabad, makao makuu ya mkoa wa Telangana kusini mwa India, ambapo pia amewataka Waislamu kote duniani kuiunga mkono kadhia ya Palestina.

Huku akishiria namna Mtume Muhammad SAW alivyokuwa akisisitiza mara kwa mara kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu pasina kujali tofauti zao za kimadhehebu, Rais wa Iran amewataka Waislamu kukumbuka kila mara kuuombea umoja wao.

Amesema, "Iwapo jamii moja ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu inakabiliwa na changamoto fulani, basi ni kutokana na Waislamu kupuuza au kutofanyia kazi mafundisho halisi ya dini yao." 

Rais Rouhania akipokewa na viongozi wa mji wa Hyderabad

Kadhalika kwa mara nyingine tena Rais wa Iran amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuitambua Quds Tukufu kuwa eti mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, chokochoko ambayo imelaaniwa vikali kote duniani.

Aidha Rais Hassan Rouhani amelaani kitendo cha Washington cha kupiga marukufu raia na wakimbizi kutoka nchi sita zenye iddadi kubwa ya Waislamu kuingia nchini Marekani na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa chuki za maadui dhidi ya Waislamu.

Rais wa Iran aliwasili nchini India jana Alkhamisi kwa ziara rasmi ya kikazi ya siku tatu, kufuatia mualiko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Narendra Modi, ambaye wanatazamiwa kukutana kesho Jumamosi, pamoja na Rais wa India, Ram Nath Kovind. 

Dakta Rouhani ambaye ameandamana na Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hii, mapema leo alikutana na Waislamu wa mji wa Hyderabad, ambapo alitahadharisha kuhusu njama za Wamagharibi za kujaribu kupanda mbegu za uhasama miongoni mwa Waislamu, kwa kuunda makundi ya kigaidi na kitakfiri.

Dakta Rouhani alipotembelea baadhi ya maeneo yenye athari za kihistoria nchini India