EU: Vitongoji vyote vya walowezi wa Kiyahudi ni haramu
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema vitongoji vyote vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni haramu na vizingiti vya kupatikana amani Mashariki ya Kati.
Akihutubu katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa EU na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Brussels, Mogherini amesema ni muhali kupatikana amani ya kudumu Mashariki ya Kati iwapo Israel itaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa upande wake, Ayman al-Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan amesema suluhisho pekee la mgogoro uliopo ni kuhakikisha kuwa Quds Tukufu inatambulika kuwa mji mkuu wa Taifa la Palestina.
Mwezi uliopita, utawala khabithi wa Israel uliafiki pendekezo la ujenzi za nyumba zaidi ya 1000 katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, mbali na mpango wa ujenzi wa nyumba zingine 2500 katika maeneo tofauti ya Palestina.
Hatua hiyo inafanyika katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Disemba 2016 lilipitisha azimio ambalo linautaka utawala wa Israel kuhitimisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina.