Putin: Crimea kamwe haitarejeshwa kwa Ukraine
Rais wa Russia amesema kuwa nchi hiyo kamwe haitairejesha Crimea kwa Ukraine.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Russia One, Rais Vladimir Putin amebainisha kuwa Russia kwa hali yoyote ile haitakirejesha kisiwa cha Crimea kwa Ukraine na kwamba jambo hilo haliwezekani. Rais wa Russia ameongeza kuwa hakuna njia ya kukikabidhi kisiwa hicho na wala hakuna uwezekano wa kutekelezwa jambo hilo. Rais Putin ameyatamka hayo katika mahojiano wiki moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais wa Russia.
Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umeiwekea Moscow vikwazo kutokana na matukio yanayoendelea huko mashariki mwa Ukraine na katika kisiwa cha Crimea. Kisiwa cha Crimea mwaka 2014 kilitangaza kuwa huru na kujitenga kwa upande mmoja na Ukraine baada ya kufanyika kura ya maoni. Kisiwa hicho kiliwasilisha ombi la kujiunga na Russia; ombi ambalo liliidhinishwa na Russia baada ya viongozi wa nchi hiyo kusaini makubaliano ya kujiunga kisiwa hicho na Russia.