Kremlin: Putin yuko tayari kukutana na Zelensky kukamilisha makubaliano ya amani
-
Rais Vladimir Putin
Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, imeeleza kuwa Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo yuko tayari kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, lakini ikiwa mkutano wao utahusu suala la kusaini makubaliano ya amani.
Dmitry Peskov ambaye ni msemaji wa Rais wa Russia ameeeleza kuwa Rais Putin amesisitiza mara kwa mara kwamba yuko tayar kukutana na Zelenskyy.
"Suala muhimu ni lengo la mkutano. Kwa nini wanapasa kukutana? Putin amesema yuko tayari kukutana na Zelenskyy wakati wowote mjini Moscow,” ameeleza Peskov katika mkutano na vyombo vya habari.
Msemaji wa Rais Putin amesema mkutano kama huo lazima utanguliwe na "kazi nzito," na kusema kuwa Ukraine haina "utashi wa kisiasa" katika muktadha huo.
Jumatano wiki hii Rais wa Ukraine aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ukraine iko tayari kwa aina yoyote ya mazungumzo, "wakati wowote," na kwamba kuanza tena mazungumzo "hakuwategemei wao."
Amesema, nchi zinazopewa kipaumbele kuwa wenyeji wa mazungumzo kati ya Russia na Ukraine ni zile ambazo ziliwahi kuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya nchi mbili akiitaja Uturuki na hasa nchi za eneo la Mashariki ya Kati.