Mar 18, 2018 16:25 UTC
  • Nchi za Asia zambana kiongozi wa Mynamar kuhusu mauaji ya Warohingya

Viongozi wa nchi za Asia na Australia wamemjia juu kiongozi wa Myanmar kutokana na kutochukua hatua za maana serikali yake kukomesha wimbi la mauaji ya Waislamu wa jamii ya Rohingya mkoani Rakhine.

Viongozi wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN na Australia waliokutana mjini Sydney wamemtaka Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Myanmar ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Serikali ya nchi hiyo, Aung San Suu Kyi atoe ufafanuzi kuhusu kuendelea kwa mauaji na dhulma dhidi ya Warohingya.

Najib Razak, Waziri Mkuu wa Malaysia amesema mauaji ya Waislamu wa Myanmar sio tena mgogoro wa kitaifa, bali ni suala linalohusu usalama na uthabiti wa eneo zima la Asia.

Naye Malcolm Turnbull, Waziri Mkuu wa Australia amesema leo Jumapili katika kikao cha kufunga mkutano huo wa ASEAN kuwa, kuna haja jamii ya kimataifa iache kuupuuza mgogoro wa Myanmar na ifanye hima kutafuta njia za kuupatia ufumbuzi.

Kuendelea kuuawa Waislamu wa Rohingya

Kwa upande wake, Lee Hsien Loong, Waziri Mkuu wa Singapore ambaye ndiye mwenyekiti wa mwaka huu wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN amesema jumuiya hiyo haina mamlaka ya kutosha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Myanmar na kudokeza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndilo lenye uwezo na jukumu la kutegua kitendawili cha mauaji na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa, mbali na wengine zaidi ya laki saba kulazimishwa kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh, tangu Agosti 25 mwaka jana, lilipoanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo. 

Tags