Putin: Lengo la mashambulizi ya Magharibi lilikuwa kuwasaidia magaidi
(last modified Wed, 25 Apr 2018 14:02:37 GMT )
Apr 25, 2018 14:02 UTC
  • Putin: Lengo la mashambulizi ya Magharibi lilikuwa kuwasaidia magaidi

Rais wa Russia amelitaja shambulio la makombora la nchi za Magharibi huko Syria kuwa lilitekelezwa ili kuwasaidia magaidi.

Rais Vladimir Putin wa Russia leo ametuma ujumbe katika Mkutano wa Tisa wa Usalama wa Viongozi wa Ngazi za Juu kutoka mabara matano duniani unaofanyika katika mji wa kitalii wa Sochi nchini Russia ambapo amekosoa shambulio la makombora lililotekelezwa kwa pamoja na nchi tatu za Marekani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Syria hivi karibuni. Amesema kuwa shambulio hilo dhidi ya Syria ni kinyume cha sheria na lilitekelezwa kwa maslahi ya magaidi, makundi yenye kuchupa mipaka na mataifa ajinabi yanayotenda jinai ambayo husababisha kuibuka hali ya mivutano na migogoro katika nchi mbalimbali. 

Washiriki katika Mkutano wa Tisa wa Usalama unaofanyika katika mji wa Sochi nchini Russia 

Naye Nicolai Patrushev Katibu wa Baraza la Usalama la Russia ambaye amesoma ujumbe huo wa Rais Putin katika Mkutano wa Usalama wa Sochi ameongeza kuwa baadhi ya wanachama wa jamii ya kimataifa wanafanya jitihada kupuuza misingi na sheria za kimataifa zilizoainishwa. Mkutano wa Tisa wa Usalama wa viongozi wa ngazi za juu kutoka mabara matano duniani umeanza leo huko Sochi nchini Russia na utadumu kwa muda wa siku mbili.