China: Pande zote zinapaswa kuheshimu mapatano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43966-china_pande_zote_zinapaswa_kuheshimu_mapatano_ya_jcpoa
China imesisitizia umuhimu wa pande zote husika kuendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2018 21:17 UTC
  • China: Pande zote zinapaswa kuheshimu mapatano ya JCPOA

China imesisitizia umuhimu wa pande zote husika kuendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.

Katika kikao na waandishi wa habari mji Beijing jana Jumatano, Hua Chunying, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema, pande zote za makubaliano hayo ya kimataifa yaliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2016 zinapaswa kutazama kwa taswira pana na taathira chanya na za muda mrefu za mapatano hayo, na kuyatekeleza kikamilifu na kwa moyo wa kuaminiana.

Amesema Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ndicho chombo pekee cha kimataifa chenye haki na jukumu la kusimamia mapatano hayo, na kuyatolewa hukumu.

Baadhi ya maafisa wa Iran, EU na kundi la 5+1 waliofanikisha mapatano JCPOA Julai 2015

Matamshi ya Hua Chunying, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China yanaonekana ni jibu lisilo la moja kwa moja kwa matamshi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye Jumatatu iliyopita aliweka kadamnasi kile alichodai kuwa ni ithibati ya kuoonyesha kuwa Iran inaendesha kwa siri mpango wa kumiliki silaha za nyuklia. 

Aidha msimamo huu wa China umetolewa siku chache kabla ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza iwapo nchi hiyo itajiondoa kwenye mapatano hayo au la. Trump ambaye amekuwa akiyaponda mapatano hayo anatazamiwa kutoa tangazo hilo Mei 12.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ina machaguo kadhaa ya kuchukua iwapo Marekani itajiondoa kwenye mapatano hayo ya nyuklia, ikiwemo kujiondoa kwenye mkataba wa NPT wa kuzuia utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa silaha za atomiki, sambamba na kuanzisha upya shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani lakini kwa kasi ya juu.