Venezuela yawatimua wanadiplomasia wa Marekani
(last modified Wed, 23 May 2018 07:21:23 GMT )
May 23, 2018 07:21 UTC
  • Venezuela yawatimua wanadiplomasia wa Marekani

Venezuela imewafukuza nchini wanadiplomasia wawili wa ngazi za juu wa Marekani, ikiwa ni radiamali ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini ya kujibu uhasama mpya wa Washington wa kushadidisha vikwazo dhidi yake.

Akitoa tangazo hilo jana Jumanne kwa njia ya televisheni, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amewataka wanadiplomasia hao kuondoka nchini humo ndani ya masaa 48.

Amesema balozi mdogo wa Marekani nchini humo, Todd Robinson na naibu wake Brian Naranjo watakuwa nchini humo kinyume cha sheria iwapo hawatakuwa wameondoka baada ya kupita muda huo.

Rais Maduro ameongeza kwa kusema, "Ninalaani kwa nguvu zote vikwazo vyote dhidi ya watu wa Jamhuri ya Venezuela, kwa sababu vinalenga kuliumiza taifa hili."

Trump na Maduro

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Venezuela siku ya Jumatatu kutokana na ushindi wa Maduro katika uchaguzi wa rais wa Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela ilivitaja vikwazo hivyo vipya dhidi ya nchi hiyo kama jinai dhidi ya binadamu.

Hivi karibuni, Venezuela ilisema Marekani inaendeleza 'ugaidi wa kisaikolojia' dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini, huku ikimtaja Trump kuwa mtu anayejifanya 'bepari wa dunia', baada ya Washington kuijumuisha Caracas katika orodha ya nchi nane ambazo raia wao wamepigwa marufuku kuingia Marekani.

Tags