Uholanzi kufanya mashindano ya vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45792-uholanzi_kufanya_mashindano_ya_vibonzo_vya_kumvunjia_heshima_mtume_muhammad_saw
Kiongozi wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Uholanzi amepewa kibali cha kuandaa mashindano ya kuwasilisha vibonzo vya kumvunjia heshimu Mtume Muhammad SAW.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2018 02:53 UTC
  • Uholanzi kufanya mashindano ya vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

Kiongozi wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Uholanzi amepewa kibali cha kuandaa mashindano ya kuwasilisha vibonzo vya kumvunjia heshimu Mtume Muhammad SAW.

Geert Wilders ametoa tangazo hilo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo amebainisha kuwa: "Idara ya Kupambana na Ugaidi ya Uholanzi NCTV imetupa kibali cha kuandaa mashindano ya vibonzo vya Muhammad katika ofisi yangu yenye usalama wa kutosha kwenye majengo ya Bunge baadaye mwaka huu."

Mwaka 2016, mbunge huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Uholanzi alipatikana na hatia ya kuwatusi watu wenye asili ya Morocco na kuwabagua kwa misingi ya dini zao.

Wilders amewahi kusema huko nyuma kuwa, iwapo atafanikiwa kuwa Waziri Mkuu wa Uholanzi, atapiga marufuku Qur'ani Tukufu na kufunga misikiti yote nchini humo.

Kabla ya hapo Geert Wilders alikifananisha kitabu hicho cha mbinguni na kitabu cha 'Vita Vyangu' kilichoandikwa na Adolf Hitler.

Waislamu nchini Uholanzi

Chama cha mwanasiasa huyo chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, kinaendelea kupata umashuhuri nchini Uholanzi kutokana na kujikita kwenye hisia za chuki dhidi ya wageni na Waislamu nchini humo na kote barani Ulaya.

Februari mwaka huu na katika kuendeleza vitendo vya unyanyasaji na chuki dhidi ya Waislamu, watu wenye chuki za kidini waliuchoma moto msikiti mmoja katika mji wa Drachten wa kaskazini mwa Uholanzi.