Wahajiri Milioni 2.5 walisafrishwa kimagendo mwaka 2016
Wahajiri wasiopungua 2.5 walisafirishwa kimagendo mwaka 2016 ambapo wafanya magendo ya binadamu waliohusika walipata faida ya dola bilioni saba za Kimarekani.
Hayo yamebainika katika ripoti ya kwanza duniani ya magendo ya wahajiri ambayo imechapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).
Ripoti hiyo imesema kuwa, usafirishaji kimagendo wahajiri hufanyika katika maeneo yote ya dunia na pato haramu la dola bilioni saba litokanalo na magendo hiyo ni sawa na bajeti ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Ulaya ya mwaka 2016.
Aidha ripoti hiyo imefichua kuwa kuna njia 30 kuu ambazo hutumiwa katika kuwasafirisha wahajiri kimagendo ambapo wakimbizi wengi hulazimika kutumia njia hizo kukimbia masaibu au vita katika nchi zao. Takwimu zinaoneysha kuwa watoto ni waathirika wakubwa wa njia hizo za kimagendo ambapo mwaka 2016 pekee, watoto 34,000 waliokuwa wakisafiri peke yao au bila wazazi wao waliingia Ulaya kupitia Ugiriki, Italia, Bulgaria na Uhispania.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IMO, linasema maelfu ya wahajiri hupoteza maisha kabla ya kufika nchi walizokusudia. Wengi huzama baharini na wengine hupoteza maisha katika ajali au kutokana na hali mbaya ya hewa. Baharini ya Mediterranea ndio njia mbaya zaidi na huchangia karibu asilimia 50 ya vifo vyote vya wahajiri.