Jul 01, 2018 07:53 UTC
  • Ubelgiji yasimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia

Mahakama ya Juu ya Ubelgiji imesimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia ikisema kuwa serikali ya nchi hiyo ilishindwa kutathmini rekodi mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu ya utawala huo wa kifalme kabla ya kutoa leseni za kuruhusu mauzo hayo.

Mahakama hiyo imesimamisha leseni nane za mauzo ya silaha, uamuzi ambao umeiathiri pakubwa kampuni ya silaha ya FN Herstal iliyoko katika eneo la Wallonia ambalo wakazi wake wengi wanazungumza Kifaransa.

Kampuni hiyo ambayo pia inajulikana kama Fabrique Nationale mwaka jana iliiuzia Saudia silaha zilizokuwa na thamani ya dola milioni 179. Miaka miwili kabla hapo, Riyadh ilinunua silaha zilizokuwa na thamani ya dola milioni 672 kutoka kampuni hiyo. 

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni mashirika mawili ya kutetea haki za binadamu ya Droit Solidarite na Aser yaliipa Ufaransa makataa ya miezi miwili iache kuuuzia silaha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, vinginevyo yataichukulia hatua za kisheria.

Nchi mbalimbali za Ulaya zimekuwa zikipinga kuuziwa silaha Saudia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekuwa likisisitiza kuwa, mauzo ya silaha za nchi za Magharibi kwa Saudia na waitifaki wake zinazotumika katika hujuma dhidi ya Yemen ni kejeli kwa Makubaliano ya Kimataifa ya Uuzaji wa Silaha.

Saudia kwa kushirikiana na Marekani,  utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya taifa masikini la Yemen hapo mwezi Machi 2015, ambapo mbali na kuua makumi ya maelfu ya watu, yameharibu miundombinu ya nchi hiyo maskini.

Tags