Kusimamishwa uuzaji silaha za Ubelgiji kwa Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46502-kusimamishwa_uuzaji_silaha_za_ubelgiji_kwa_saudi_arabia
Kufuatia hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kuendelea kuishambulia kijeshi Yemen, Baraza la Kiserikali la Ubelgiji, limetoa amri ya kusimamishwa uuzaji silaha wa nchi hiyo kwa Riyadh.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 01, 2018 22:01 UTC
  • Kusimamishwa uuzaji silaha za Ubelgiji kwa Saudi Arabia

Kufuatia hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kuendelea kuishambulia kijeshi Yemen, Baraza la Kiserikali la Ubelgiji, limetoa amri ya kusimamishwa uuzaji silaha wa nchi hiyo kwa Riyadh.

Kwa mujibu wa amri hiyo ambayo imetolewa kufuatia malalamiko ya makundi ya haki za binaadamu, jumla ya leseni nane za mauzo ya silaha kati ya kampuni ya kuzalisha silaha ya FN Herstal ya nchi hiyo pamoja na Saudia, zitabatlishwa hivi karibuni. Mwaka jana 2017 kampuni ya kutengeneza silaha ya FN Herstal, iliiuzia Saudia silaha za thamani ya karibu Euro milioni 153. Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Saudi Arabia imegeuka na kuwa mnunuzi mkubwa wa silaha duniani. Ununuzi huo mkubwa wa silaha umeongezeka maradufu tokea aingie madarakani Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud sambamba na Riyadh kushadidisha migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati kukiwemo kuanzisha vita vya kivamizi dhidi ya Yemen.

Tangu kuingia madarakani watawala hawa, Saudia imegeuka na kuwa mnunuzi mkubwa wa silaha duniani.

Mbali na Saudia, Imarati, ambaye ni mshirika mkubwa wa watawala wa Riyadh, inahesabika pia kuwa miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa silaha baada ya Saudia. Silaha hizo si tu kwamba zinatumika katika kuishambulia nchi masikini ya Yemen, lakini pia zinatumika katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na ukufurishaji yanayoendesha harakati zao katika eneo, likiwemo genge hatari la Daesh (ISIS), Jab’hatu Nusra na mengine mengi. Kufuatia hali hiyo, ‘Kituo cha Utafiti wa Silaha’ kimefichua kwamba sehemu kubwa ya silaha ambazo zilikabidhiwa kundi la kigaidi la Daesh, zilitoka Marekani na Saudi Arabia. Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, silaha hizo zilikabidhiwa wanachama wa kundi hilo kwa njia ya siri ambapo Washington na Riyadh zilikuwa na nafasi kubwa katika kuwafikishia magaidi hao silaha hizo nchini Iraq na Syria.

Sehemu kubwa ya fedha za Saudia zinatumika kununulia silaha na kuwahonga viongozi wa asasi za kimataifa

Akthari ya nchi za Ulaya zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Uhispania ni miongoni mwa wadhamini wa silaha kwa Saudia na waitifaki wake. Hii ni katika hali ambayo kushtadi vita nchini Yemen na kusababisha mauaji ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wasio na hatia, kumeibua wimbi kubwa la malalamiko kutoka kwa makundi ya watetezi wa haki za binaadamu katika nchi tofauti za Ulaya. Kwa mujibu wa makundi hayo, hatua ya akthari ya nchi za Ulaya na Marekani ya kufunga mikataba ya mauziano ya silaha na Saudia na washirika wake, ni sababu ya kuongezeka vita na kuibuka mizozo katika eneo hususan nchini Yemen na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS). Kuhusiana na suala hilo, Andrew Smith, Msemaji wa Taasisi Inayoendesha Kampeni ya Kupinga Biashara ya Silaha anasema: “Mashambulizi ya Saudia nchini Yemen hadi sasa yamesababisha mauaji ya maelfu ya raia wa nchi hiyo, na hivyo kuwa moja ya maafa makubwa zaidi ya kibinaadamu duniani.

Watu wakiandamana kupinga ukatili wa Saudia

Pamoja na hali hiyo, lakini serikali za Magharibi zimeendelea kuiunga mkono Riyadh na kuupatia silaha utawala wa kifalme wa Saudia.” Mwisho wa kunukuu. Siasa hizo za madola ya Magharibi zinatekelezwa katika hali ambayo akthari ya viongozi wa nchi hizo wamekuwa wakitoa matamshi ya undumakuwili kuhusiana na suala la haki za binaadamu ambapo kwa upande mmoja wanalaani vita na mauaji na kwa upande mwingine kuiuzia silaha Saudia kwa ajili ya kutekeleza mauaji ya kutisha nchini Yemen. Katika uwanja huo, kuongezeka wimbi la malalamiko ya watu na makundi ya kutetea haki za binaadamu kote duniani dhidi ya siasa hizo za kuiuzia silaha Riyadh na washirika wake sambamba na jitihada za kisheria zinazofanywa kwa ajili ya kuzuia mauzo hayo ya silaha, ni hatua kubwa yenye lengo la kuzishinikiza serikali za Magharibi kuacha kuziuzia silaha tawala kandamizi za Kiarabu katika eneo.