Saudia yasimamisha safari za ndege kwenda Canada na mabadilishano ya wanafunzi
Kufuatia hatua ya serikali ya Canada kuukosoa utawala wa Aal-Saudia kutokana na utawala huo kuzidisha kamatakamata dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo, shirika la ndege la Saudia limetangaza kusimamisha safari zake kwenda au kutokka Canada.
Kadhalika serikali ya Riyadh imetangaza kwamba, kutokana na hatua ya serikali ya Ottawa ya kukosoa hali ya haki za binadamu nchini Saudia mbali na kutimuliwa balozi wa Canada, imekatana mahusiano yote ya kibiashara na kusimamiasha miradi yote ya uwekezaji nchini Saudia. Kama hiyo haitoshi Saudia pia imetangaza kufuta nafasi za masomo kwa ajili ya wanafunzi wa Saudia wanaosoma nchini Canada. Katika hilo Saudia imesema, mabadilishano ya wanafunzi kati yake na Canada na nafasi zote za masomo imeamua kuyasimamisha.
Mubarakk al-Asimi, Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Saudia ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Riyadh amesimamisha mahusiano ya kielimu na Canada na badala yake itawatuma wanafunzi wake kwenda nchi kama vile Uingereza, Marekani, Australia na New Zealand.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia, mapema jana asubuhi ilimpa balozi wa Canada muda wa masaa 24 kuondoka nchini Saudi Arabia kama njia ya kulalamikia hatua ya serikali ya Canada ya kusema kuwa ina wasiwasi kuhusu hatua zilizochukuliwa nchini Saudia za kuwatia mbaroni wanaharakati wa asasi za kijamii na wapigania haki za wanawake.