Maelfu ya Waislamu China waandamana kupinga kubomolewa msikiti
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47357-maelfu_ya_waislamu_china_waandamana_kupinga_kubomolewa_msikiti
Maelfu ya Waislamu nchini China wamefanya maandamano kupinga hatua ya serikali ya kutaka kubomolewa msikiti kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 10, 2018 12:15 UTC
  • Maelfu ya Waislamu China waandamana kupinga kubomolewa msikiti

Maelfu ya Waislamu nchini China wamefanya maandamano kupinga hatua ya serikali ya kutaka kubomolewa msikiti kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Maandamano hayo yamefanyika katika mji wa Weizhou wa wilaya ya Haicheng, kufuatia hatua ya viongozi wa serikali ya eneo lenye mamlaka ya ndani la Ningxia Hui, kutaka kubomoa msikiti uliojengwa hivi karibuni.

Maandamano hayo yamewalazimisha viongozi wa mji huo kurudi nyuma. Inaelezwa kwamba Waislamu hao walianzisha maandamano hayo baada ya Swala ya Adhuhuri mchana wa jana na kuendelea hadi usiku ambapo walikuwa wamezuguka maeneo ya msikiti huo kwa lengo la kuwazuia maafisa usalama waliokuwa wamekusudia kuizingira nyumba hiyo ya ibada.

Waislamu nchini China

Kiongozi mmoja wa serikali ya mji huo amewaambia waandamanaji kwamba, serikali imeachana na mpango wa kubomoa msikiti huo na amewataka Waislamu kuondoka eneo hilo na kurejea majumbani mwao. Kiongozi huyo ameelezea azma ya serikali ya kufanya mazungumzo na Waislamu wa eneo hilo juu ya kadhia hiyo.

Itakumbukwa kuwa tarehe tatu mwezi huu, serikali ya mji wa Weizhou ilitoa taarifa kwamba, kwa kuzingatia kuwa msikiti huo haukuwa na vibali utatakiwa kubomolewa. Takwimu rasmi za serikali ya China zinaonyesha kwamba, idadi ya Waislamu nchini humo inakaribia milioni 23, ingawa duru zisizo rasmi zinasema idadi ya Waislamu hao nchini humo ni kati ya milioni 50 hadi 70.