Aug 15, 2018 02:35 UTC
  • Uturuki yajibu mapigo, yaziwekea vikwazo bidhaa za kielektroniki za Marekani

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametangaza kuwekewa vikwazo bidhaa za kielektroniki zinazozalishwa nchini Marekani.

Erdoğan ametoa tangazo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jumanne ya jana mjini Ankara na kusisitiza kwamba, katika kukabiliana na siasa za kiuchumi zisizo na busara wala mantiki za Rais Donald Trump wa Marekani, kuanzia sasa Uturuki itaanza kuzalisha bidhaa zilizokuwa zinaingizwa kwa fedha za kigeni nchini humo sambamba na kuziuza bidhaa hizo nchi nyingine. Sambamba na kubainisha kwamba, siasa za kiuchumi za Trump dhidi ya Uturuki haziendani na akili wala mantiki yoyote ameongeza kwamba, viongozi wa Marekani wakati wanapohisi kuwa hawana uwezo wa kuitwisha matakwa yao Uturuki, hutumia nguvu ya kijeshi na kuibua machafuko ya kijamii na kisiasa kama silaha pekee kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki

Kadhalika Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amefafanua kuwa, serikali ya Ankara inakusudia kuwapokea kuliko wakati mwingine wowote ule wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini humo. Mahusiano kati ya Marekani na Uturuki yamevurugika katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na masuala tofauti, ikiwemo udhibiti wa eneo la Manbij, kaskazini mwa Syria, hatua ya Washington ya kukataa kumkabidhi Fethullah Gülen kwa serikali ya Ankara, hatua ya serikali ya Uturuki kumshikilia Andrew Brunson, padri wa Kimarekani anayetuhumiwa kufanya ujasusi na kushirikiana na magaidi nchini Uturuki, hatua ya Marekani kuwawekea vikwazo Mawaziri wa Sheria na Mambo ya Ndani wa Uturuki na pia hatua ya Marekani kuzipandishia ushuru wa forodha bidhaa za chuma na aluminiamu za Uturuki.

Tags