UN Yataka viongozi wa duinia kulinda watu walionaswa kwenye mizozo
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa viongozi wa dunia kufanya kila wawezalo kulinda watu walionaswa kwenye mizozo.
Kupitia ujumbe wake kwa munasaba wa siku ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa mizozo inaongezeka, raia wanaolengwa kwenye mizozo vivyo hivyo, hali kadhalika wale wanaofunga safari kwenda kuwasaidia.
Ametolea mfano kuwa miaka 15 tangu shambulio dhidi ya ofisi za Umoja wa Mataifa huko Baghdad nchini Iraq lililosababisha vifo vya wafanyakazi 22, idadi ya wafanyakazi waliouawa, kujeruhiwa au kushikiliwa wakiwa kazini ni zaidi ya 4000.
“Kiwango hicho kinamaanisha kuwa wastani wa wafanyakazi 300 wa kutoa huduma za misaada wanauawa kila mwaka,” amesema Katibu Mkuu.
Guterres amesema raia nao hawako salama kwani kwenye maeneo ya mizozo, wanauawa au kuachwa na ulemavu katika mashambulizi ya makusudi au yasiyochagua popote.
Aidha katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulibaini kuwa zaidi ya raia 26,000 waliuawa kwenye mapigano katika nchi sita ambazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Iraq, Somalia na Yemen. Ni kutokana na mapigano hayo, amesema Katibu Mkuu, ulimwenguni kote idadi ya watu waliofurushwa makwao ni zaidi ya milioni 65, watoto nao wakitumikishwa vitani.
Siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa kibinadamu ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kuenzi watendaji wa chombo hicho waliouawa wakati wa mashambulizi dhidi ya makao makuu ya UN huko Baghdad, Iraq mwaka 2005.